Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yaona matumaini kuhusu vita dhidi ya uvuvi haramu

FAO yaona matumaini kuhusu vita dhidi ya uvuvi haramu

Idadi ya nchi zinazokubali kupambana na uvuvi haramu inaongezeka, limesema Shirika la Chakula na Kilimo FAO likitumai kwamba nchi nyingi barani Afrika zitakubali kuridhia mkataba wa kimataifa unaowezesha bandari kuzuia na kudhibiti uvuvi haramu.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, FAO imesema asilimia 15 ya samaki zinazovuliwa duniani ni kupitia uvuvi haramu, yaani tani milioni 26, ikiwa ni changamoto kubwa kwa uchumi wa nchi husika, pia athari kwa uendelevu wa rasilimali na uhakika wa chakula.

Mkataba wa kimataifa wa kuzuia na kudhibiti uvuvi haramu kupitia bandari utawezesha bandari kuimarisha ufuatiliaji wa boti za wavuvi, imeongeza FAO, ikisema aidha itaruhusu mamlaka za bandari kukataza boti zinazovua samaki kwa njia haramu kutia nanga.

Hata hivyo, FAO imesema mkataba huo uliosainiwa mwaka 2009 hautatekelezwa mpaka nchi 25 ziuridhie. Hadi sasa, nchi 12 tu zimetimiza utaratibu huo, zikiwemo Gabon na Msumbiji.

Licha ya hayo, FAO imeeleza matumaini yake baada ya kuitisha mkutano wa kikanda nchini Capo Verde mwezi huu, ambapo nchi nyingi za Afrika Magharibi zimeonyesha utayari wao wa kuridhia mkataba huo.