Kilimo hai ni mustakhabali wa kilimo barani Afrika:UNEP

Kilimo hai ni mustakhabali wa kilimo barani Afrika:UNEP

Kutunza mifumo ya ekolojia iliyopo barani Afrika ni njia endelevu ya kuhakikishia uhakika wa chakula kwa watu, amesema leo mratibu wa maswala ya mabadiliko ya tabianchi kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira, UNEP, Richard Munang. Taarifa kamili na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Bwana Munang amesema hayo wakati watalaam wa maswala ya kilimo na uhakika wa chakula wakikutana mjini Nairobi kujadili utohozi wa mifumo ya ekolojia kwa ajili ya uhakika wa chakula, kwenye mkutano wa siku mbili ulioandaliwa na UNEP.

Bwana Munang amesema matumizi ya viuadudu na mbolea ya kemikali vinaharibu udongo na mali asili na hivyo kuathiri uzalishaji wa chakula kwa kipindi cha muda mrefu. Ameongeza kwamba kilimo hai na nyenzo asili ya kilimo ndio njia bora ya kuendeleza sekta ya kilimo barani Afrika:

“ Kwa mtazamo wa UNEP, ushauri kwa serikali ni kwamba kutunza mifumo ya ekolojia kwenye sekta ya kilimo kutazalisha ajira zaidi kwa sababu ni endelevu kuliko mitazamo ya muda mfupi ambayo inategemea mbolea isio hai. Kwa hiyo, kuunda sera ambazo hasa zinahusisha vijana kufadhiliwa ili kuweza kutumia nyenzo hizo hai zinazolinda mifumo ya ekolojia ni muhimu sana.” 

Kwa mujibu wa UNEP, ongezeko la asilimia 10 la ufanisi wa uzalishaji kwenye sekta  ya kilimo linasababisha kiwango cha umaskini kupungua kwa asilimia 7, Bwana Munang akisema jitihada kwenye sekta ya kilimo ndio njia pekee ya kukabiliana na ongezeko kubwa la idadi ya watu linalotarajiwa barani Afrika kwenye kipindi cha miaka ijayo.