Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Urusi yapinga azimio la kuanzisha mahakama kuhusu ndege ye Malaysia MH 17

Urusi yapinga azimio la kuanzisha mahakama kuhusu ndege ye Malaysia MH 17

Urusi imetumia kura yake ya turufu leo, kupinga kupitishwa azimio la kutaka iwekwe mahakama ya kimataifa ya kuwashtaki watu waliotekeleza uhalifu uliosababisha kutunguliwa kwa ndege ya Malaysia ya MH17.

Uchina, Angola na Venezuela ni nchi zingine ambazo hazikupinga au kuunga mkono azimio hilo, ambalo limeungwa mkono na wanachama 11 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Pamoja na kutaka izinduliwe mahakama ya kushitaki wahalifu walioitungua ndege ya MH17, azimio hilo lilitaka uharakishwe uchunguzi kuhusu kilichosababisha ajali hiyo ya ndege, bila kuvuruga ubora wa uchunguzi huo.

Rasimu ya azimio hilo iliandaliwa na Malaysia, ambayo Waziri wake wa masuala ya Usafiri, Liow Tiong Lai amekuwa na haya ya kusema, mara baada ya kura ya azimio hilo:

“Kwa masikitiko, mwaka mmoja tangu kupitishwa kwa kauli moja kwa azimio la Baraza la Usalama namba 2166, Baraza sasa linapiga hatua nyuma kwa kupeleka ujumbe mbaya kwa familia za wahanga na wapenzi wao. Badala ya kutuma ujumbe wa kuunga mkono haki na uwajibikaji, tunatuma ujumbe hatari wa ukwepaji sheria kwa watekelezaji wa uhalifu huu mbaya, na pia kuweka hatarini usalama wa usafiri wa umma kupitia maeneo ya mizozo katika siku zijazo.”

Amesema Baraza hilo pia limeshindwa kutekeleza azimio namba 2166, ambalo lilitaka wote waliohusika wawajibishwe, na kwamba nchi zote zishirikiane katika juhudi za uwajibishaji.