Skip to main content

IMF yapongeza mafanikio ya Somalia kiuchumi

IMF yapongeza mafanikio ya Somalia kiuchumi

Baada ya miaka 25 ya vurugu nchini Somalia, Shirika la Fedha Duniani, IMF limezindua leo ripoti yake ya kwanza kuhusu hali ya uchumi nchini humo, likielezea kuwa Somalia imepiga hatua kubwa katika kurejesha ukuaji wa uchumi.

Akihojiwa na idhaa hii, Rogerio Zandamela, mkuu wa ujumbe wa IMF nchini Somalia, amesema licha ya umaskini na matatizo ya kiusalama na kibinadamu yanayokumba nchi hiyo, ukuaji wa uchumi nchini Somalia umefika asilimia 3.7 mwaka 2014, huku ongezeko la bei ya bidhaa likidhibitiwa.

Ameongeza kuwa ukuaji wa uchumi umesababishwa na uuzaji wa mifugo na samaki, ukuaji wa sekta binafsi katika sekta za ujenzi na mawasiliano, wasomali wengi waliokuwa ughaibuni wakirudi kuwekeza nchini humo.

Hata hivyo Bwana Zandamela amesema bado changamoto ni nyingi, serikali ya Somalia ikidaiwa pesa na IMF na mashirika mengine, huku ikishindwa kufadhili matumizi yake. Ameeleza mapendekezo ya IMF:

(Sauti ya Rogerio Zandamela)

“ Nchini Somalia kama kwenye nchi nyingine kadhaa zilizodhoofika kiuchumi tunazofanya kazi nazo, mamlaka imara na utawala bora ni misingi ya kurejesha uaminifu wa raia kwa serikali.”