Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo wa Syria ni ishara ya aibu ya migawanyo na kufeli kwa jamii ya kimataifa- Ban

Mzozo wa Syria ni ishara ya aibu ya migawanyo na kufeli kwa jamii ya kimataifa- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameliambia Baraza la Usalama leo kwamba baada ya miaka minne ya uchinjaji, mzozo wa Syria ni ishara ya aibu ya mgawanyiko na kufeli kwa jamii ya kimataifa. Taarifa kamili na Priscilla Lecomte

(Taarifa ya Priscilla)

Akilihutubia Baraza la Usalama ambalo limekutana leo kuhusu Syria, Katibu Mkuu amesema amesikitishwa sana kwamba maazimio ya Baraza hilo kuhusu Syria hayajatekelezwa- iwe katika kumaliza machafuko au katika kumaliza mateso ya kibinadamu au kukabiliana na ugaidi na wapiganaji wa kigeni.

“Syria ndio mzozo mkubwa zaidi duniani wa kibinadamu. Raia wa Syria wapatao robo ya milioni wameuawa. Takriban nusu ya idadi ya raia wa Syria- wanaume, wanawake na watoto milioni 12, wamelazimika kukimbia makwao. Halaiki ya watu wamevuka mpaka, na sasa Uturuki, Lebanon, Jordan na Iraq zinawapa hifadhi idadi inayoongezeka ya wakimbizi, huku WaSyria wengi wakifanya safari hatarishi kuvuka Bahari ya Mediterenia kwa kutumia boti za kifo.”

Ban ametoa wito kwa Baraza la Usalama, nchi jirani za Syria na wafadhili wa kikanda kwa pande kinzani katika mzozo wa Syria zikomeshe usambazaji wa silaha na wapiganaji wa kigeni kuingia nchini.

“Hali nchini Syria haikubaliki. Tusiwatelekeze watu wa Syria katika lindi la kukata tamaa hata zaidi. Tusihukumu ukanda mzima kusalia katika machafuko yasiyo na mwisho. Baraza hili lina jukumu la kuunga mkono mchakato wa kisiasa kwa kuchukua hatua kumaliza mzozo.”