Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Somalia waongezwa kwa mwaka moja

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Somalia waongezwa kwa mwaka moja

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha leo kwa kauli moja azimio la kuongeza muda wa mamlaka za Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNSOM hadi tarehe 30, Machi, mwaka 2016. Azimio limesisitiza jukumu la kisiasa la UNSOM, hasa wakati huu ambapo Somalia inatarajia kuandaa uchaguzi mwaka 2016.

Aidha wanachama wa Baraza hilo wameruhusu Muungano wa Afrika kuongeza muda wa Ujumbe wake nchini humo AMISOM hali tarehe 30, Mei, mwaka 2016 idadi ya wanajeshi wake ikiwa haipaswi kuzidi 22,126.

Baraza la Usalama limeiruhusu AMISOM kuchukua hatua zozote ili kulisaidia jeshi la Somalia katika kupambana na kundi la kigaidi la Al-Shabab, kwa kuheshimu haki ya kimataifa ya kibinadamu.

Kadhalika azimio hilo linauomba Muungano wa Afrika kuongeza ufanisi wa AMISOM kwa kuimarisha uongozi wake na kuunda vikosi maalum vya wanajeshi.