Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

SYRIA: Mkuu wa OCHA ashtushwa na hali ya kibinadamu

SYRIA: Mkuu wa OCHA ashtushwa na hali ya kibinadamu

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa maswala ya kibinadamu, Stephen O’Brien, amelieleza leo Baraza la Usalama kwamba hali ya kibinadamu inazidi kuzorota nchini Syria, huku watu milioni 12.2 wakihitaji msaada wa kibinadamu.

Bwana O’Brien amesema usalama wa raia unashindwa kulindwa kwenye vita hivyo vinavyodumu kwa miaka mitano, watu 220,000 wakiripotiwa kuuwawa tangu mwanzo wa mzozo huo.

(SAUTI O'BRIEN)

“ Mashambulizi ya kupindukia yasiyokuwa na lengo maalum kutoka kwa pande zote za mzozo, ikiwemo matumizi ya mabomu kwenye maeneo ya makazi ni kwa mbali sababu ya kwanza ya vifo vya raia. Makazi ya raia lakini pia soko, shule, hospitali, sehemu za ibada zinalengwa na mashambulizi. Kutokana na mashambulizi hayo makali, si vigumu kuhisi wanachopitia wasyria kutoka jamii mbali mbali. Ni uchaguzi mbaya zaidi kwao: ama kukimbia, ama kuuawa.”

Halikadhalika Bwana O’Biren amesema usambazaji wa misaada ya kimataifa unakumbwa na changamoto kadhaa, huku wahudumu wa kibinadamu 77 wakiuawa tangu mwanzo wa mzozo.