Skip to main content

Homa ya uti wa mgongo changamoto kubwa barani Afrika :WHO

Homa ya uti wa mgongo changamoto kubwa barani Afrika :WHO

Bara la Afrika liko hatarini kukumbwa na mlipuko mkubwa wa homa ya uti wa mgongo, aina ya C, limesema leo Shirika la Afya duniani WHO.

WHO pamoja na mashirika mengine imetoa wito kwa kampuni za kutengeneza madawa ili ziongeze uzalishaji wa chanjo na zipunguze bei yake. Sasa hivi bei ya chanjo kwa mtu mmoja inakaribia dola 30.

Olivier Ronveaux ni mtalaam wa magonjwa ya milipuko kwa WHO.

“ Ni vigumu kutabiri jinsi aina ya C ya homa hiyo itasambaa, lakini tulishuhudia mamia ya visa mwaka 2013, maelfu mwaka 2014, na mwaka huu tayari ni visa 12,000, kwa hiyo ni wazi kwamba ugonjwa huo unaenea. Ni vigumu kujua mwelekeo, lakini tunajaribu kutayarisha jamii na kupata chanjo kwa bei nafuu.”

Kwa mujibu wa WHO, tayari watu 800 wamefariki dunia nchini Niger na Nigeria mwaka huu kwa sababu ya homa hiyo, huku WHO ikisema akiba za chanjo milioni 5 zinahitajika ili kuweza kutokomeza mlipuko huo.

Mwaka 2010, mlipuko wa homa ya uti wa mgongo aina ya A umeweza kudhibitiwa kupitia kampeni kubwa ya chanjo.