Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maonyesho ya Norman Rockwell yaonyesha maana ya “sisi raia” kwenye Umoja wa Mataifa

Maonyesho ya Norman Rockwell yaonyesha maana ya “sisi raia” kwenye Umoja wa Mataifa

Watu wanaotembelea makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani miezi hii ya Julai na Agosti mwaka huu wataweza kushuhudia sanaa za mchoraji maarufu Norman Rockwell kutoka Marekani akichora kuhusu Umoja wa Mataifa wenyewe.

Maonyesho hayo yamefanywa kwa ajili ya kuadhimisha miaka 70 ya Umoja wa Mataifa, mchoro wa Rockwell uitwao “United Nations” wa mwaka 1953 ukisawiri wanachama wa Baraza la Usalama wakizungurukwa na watu 65 wa aina mbali mbali.

Akihojiwa na redio ya Umoja wa Mataifa, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson amesema mchoro huo ni wa kipekee.

(SAUTI ELIASSON)

“ Baraza la Usalama linawajibika kwa usalama na amani ya kimataifa. Alilchofanywa kwenye picha hiyo ya ajabu iliyochorwa na mkaa ni kuleta pamoja kazi ya diplomasia pamoja na matarajio na ndoto za watu duniani. Uzuri wa picha hiyo ni kuwa nyuma yake kuna watu karibu 60 wanaosimama ukiona sura zao zikionyesha ndoto zao, matarajio yao na wasiwasi wao wakati ule wa mwanzo wa vita baridi.”

Maonyesho hayo yamezinduliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moo akisema kuwa mchoro huo unaupa uhai mkataba wa Umoja wa Mataifa.