Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchaguzi wa rais Burundi haukuwa huru: MENUB

Uchaguzi wa rais Burundi haukuwa huru: MENUB

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kufuatilia uchaguzi nchini Burundi MENUB umetoa leo ripoti yake ya awali kuhusu uchaguzi wa rais nchini Burundi kwa kuzingatia mazingira ya sintofahamu na ghasia yaliyotawala wakati wa uchaguzi huu uliofanyika tarehe 21, Julai.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, MENUB imesema kwamba ingawa uchaguzi umefanyika kwa amani na kwa kuheshimu sheria, mazingira yaliyo nchini humo hayakuruhusu utaratibu kuwa huru, jumuishi na wa kuaminika.

MENUB imeeleza kuwa bado uhuru wa kujieleza, kuandamana kwa amani na kujumuika ambao ni misingi katika kutekeleza haki ya kupiga kura umedhoofika sana, huku ghasia ikiendelea, ingawa imepungua tangu wakati wa uchaguzi wa bunge mwezi Juni.

Aidha MENUB imesema kuwa jitihada za Rais wa Uganda Yoweri Museveni pamoja na zile za Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC hazikufanikiwa kusaidia pande zote za kisiasa nchini humo kufikia makubaliano, hasa kuhusu ratiba ya uchaguzi.

MENUB imeongeza pia kuwa vyombo vya habari vilivyoshambuliwa wakati wa maandamano havikuweza kufanya kazi, huku vyombo vya kiserikali vikiripoti kuhusu uchaguzi kwa kupendelea mgombea mmoja.

Hata hivyo MENUB imetambua kwamba warundi  wameshiriki kwenye uchaguzi kwa njia ya amani, huku utaratibu na maandalizi ya uchaguzi yakifanywa na Tume Huru ya Uchaguzi ya Kitaifa kwa kuheshimu masharti.