Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali tulivu Lebanon, lakini umakini wahitajika

Hali tulivu Lebanon, lakini umakini wahitajika

Zaidi ya miaka arubaini tangu kuanzishwa kwa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa mpito nchini Lebanon, UNIFIL, lengo kuu la operesheni hiyo ya ulinzi wa amani ni kuzuia tukio lolote la ghasia ambalo lingeweza kuibua mzozo tena baina ya Israel na Lebanon.

Mkuu wa UNIFIL, Meja Jenerali Luteni Luciano Portalano amesema hayo akihojiwa na redio ya Umoja wa Mataifa akiongeza kuwa hali ni tulivu lakini inaweza kuvurugwa muda wowote.

(SAUTI LUCIANO)

“Ni wazi kwamba kuna maeneo yanayogombaniwa na maswala ambayo hayajatatuliwa, lakini tunajaribu kusonga mbele ili kutekeleza azimio namba 1701. Itachukua muda, lakini UNIFIL ni shirika nzuri, ni nyenzo nzuri kwa serikali ya Lebanon ili kulinda amani na utulivu kusini mwa Lebanon. Na lengo kuu la Israel na Lebanon ni kuhakikishia utulivu kwenye eneo hilo.”

Azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la mwaka 2006 limeanzisha upya mamlaka ya UNIFIL kufuatia mapigano baina ya Israel na kundi la Hizbollah. Jukumu la UNIFIL ni kuhakikishia sitisho la mapigano linaheshimiwa kwenye eneo la mpakani kusini mwa Lebanon. Kwa kutimiza wajibu wake, UNIFIL ina walinda amani 10,500 na wafanyakazi 1,000, ikiwemo asilimia 3 ya wanawake.

Tarahe 28, Januari mwaka huu, mlinda amani mmoja wa UNIFIL ameuawa baada ya kupigwa risasi kwenye eneo hilo la mpakani.