Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sitisho la mapigano laanza leo Yemen

Sitisho la mapigano laanza leo Yemen

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon  amekaribisha azimio la Saudi Arabia la kusitisha mapigano kwa kipindi cha siku tano nchini Yemen, kwa ajili ya kuwezesha mashirika ya kibinadamu kufikisha misaada. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Kwenye taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Katibu Mkuu amezisihi wahouthi na pande nyingine za mzozo wa Yemen kuheshimu sitisho hilo la mapigano, akisema hilo ni la msingi kwa ajili ya raia wa Yemen wanaokumbwa na janga la kibinadamu.

Bwana Ban ameziomba pande zote kusitisha operesheni zao na kujizuia kutumia muda ule ili kuhamishia silaha au kupokonya maeneo mengine.

Aidha ameziomba pande hizo kuwezesha mashirika ya kibinadamu kusambaza misaada na kuwafikia watu wanaohitaji msaada na huduma za afya.

Kwa mujibu wa mratibu wa maswala ya kibinadamu nchini Yemen, Johannes Van der Klaauw, idadi ya wahanga wa mzozo huo imefikia 23,000.