Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa maswala ya kibinadamu aomba mapigano yasitishwe Sudan Kusini

Mkuu wa maswala ya kibinadamu aomba mapigano yasitishwe Sudan Kusini

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Misaada ya kibinadmu OCHA, Stephen O'Brien, ametimiza leo ziara yake nchini Sudan Kusini akitoa wito kwa pande zote wa kusitisha mapigano na kujenga amani endelevu, ili kusitisha mzozo wa kibinadamu nchini humo.

Bwana O'Brien amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari, akieleza kushtushwa sana na maumivu ya raia wa Sudan Kusini.

Akisema kwamba ghasia inapaswa kusimamishwa nchini humo, amewaomba viongozi wa pande zote kuwajibika ili kuhurumia raia wao na kufikia maridhiano.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na OCHA, mzozo unaoendelea kwa kipindi cha miezi 20 umesababisha watu milioni 4.6 kukumbwa na ukosefu wa chakula, huko watu milioni 2.2 wakilazimika kuhama makwao.

Bado dola bilioni moja yahitajika ili kutimiza mahitaji ya kibinadamu kwa mwaka huu pekee.