Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umuhimu wa ujuzi wa vijana katika kujiendeleza

Umuhimu wa ujuzi wa vijana katika kujiendeleza

Takriban vijana milioni 74 walikuwa wanasaka ajira mwaka 2014! Hii ni  kulingana na ripoti ya Shirika la kazi duniani ILO. Takwimu za ILO na Shirika la chakula duniani FAO mwaka 2013 zinasema kwamba vijana wanawakilisha asilimia 25% ya wafanyakazi lakini wanajumuisha asilimia 40% ya watu wasiokuwa na ajira.Ili kuimarisha uelewa kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika ukuzaji wa ujuzi wa vijana,  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeratibu Julai 15 kama siku ya ujuzi wa vijana kimataifa.Siku hii imeadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka huu wa 2015.

Katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku hiyo mapema mwezi huu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema wakati kote duniani vijana wakiwa na fursa ya elimu kuliko siku za nyuma, bado vijana barubaru milioni 75 hawako shuleni hatua inayotishia upatikanaji wa ujuzi wanaohitaji.Huku idadi ya wanaosaka kazi ikitarajiwa kuongezeka maradufu katika nchi zinazoendelea hususan zilizoko chini mwa jangwa la Afrika kati ya mwaka 2015 hadi 2050, ukosefu wa ajira kwa vijana unasalia kuwa changamoto, lakini ujuzi wanaoupata ni muarobaini kwa changamaoto hiyo.Je hali ikoje nchini Kenya? Tuungane na Geoffrey Onditi wa Radio washirika KBC, Kenya katika makala hii.