Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban apongeza Burundi kwa uchaguzi wa amani, ataka majadiliano yaendelee.

Ban apongeza Burundi kwa uchaguzi wa amani, ataka majadiliano yaendelee.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amepongeza hatua ya Burundi kuendesha uchaguzi wa Rais kwa amani mnamo Julai 21, na kutaka pande zote kusalia tulivu pamoja na kurejea hima katika majadiliano jumuishi ya kisiasa, ili kutatua tofauti zao huku pia wakishughulikia changamoto zinazokabili nchi. Taarifa kamili na Joseph Msami. (Taarifa Msami)

Tamko la Katibu Mkuu linakuja wakati huu ambapo nchi hiyo iko katika zoezi la kuhesabu kura. Taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu inasema kuwa Bwana Ban,  amezikumbusha mamlaka majukumu ya kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia na kukomesha machafuko zaidi  pamoaj na kuwajibika iwapo kutakuwa na vitendo vyovyote vya uvunjifu wa haki za binadamu.

Amekarii wito wake wa kutaka pande husika nchini Burundi kuweka mbele maslahi ya taifa kwa kujihusisha kwa imani katika majadilaino ya kisiasa na kudhamiria kutekeleza waraka wa  mkutano wa jumuiya ya Afrika Mashariki EAC yanayowezeshwa na Rais wa Uganda Yoweri Museveni  na kuongeza kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kufanyakazi na EAC na Muungano wa Afrika AU katika kupatia suluhu la kudumu Burundi.

Katika muktadha huo Katibu Mkuu amekaribisha uwepo wa waaangalizi wa haki za binadamu na wataalamu wa kijeshi kutoka AU,  ili kusaidia kukomesha kuendeela kwa machafuko  na kuwezesha sulusu la amani katika mgogoro unaoikumba Burundi.