Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tufanye kila tuwezalo kuulinda uhai wa raia Sudan Kusini- O’Brien

Tufanye kila tuwezalo kuulinda uhai wa raia Sudan Kusini- O’Brien

Msaidizi mpya wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura, Stephen O'Brien, ametoa wito wa kufanya kila liwezekanalo kuyalinda maisha ya raia nchini Sudan Kusini.

Bwana O’Brien ambaye yupo katika ziara ya siku nne nchini Sudan Kusini kujionea hali ya kibinadamu, amekuwa akikutana na wakimbizi wa ndani, ambao wamekimbia makwao kufuatia mapigano yaliyozuka mnamo Disemba mwaka 2013.

Baada ya kukutana na baadhi ya wanawake wakimbizi wa ndani, Mkuu huyo wa Shirika la OCHA amesema juhudi zote zinapaswa kufanywa ili kurejesha matumaini na ahadi ya kuheshimiana, pamoja na kuishi chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu.

"Ni muhimu tutoe ujumbe kuwa, kilicho muhimu zaidi ni thamani ya uhai wa mwanadamu, na kwamba tunapaswa kufanya kila tuwezalo kuwalinda raia wasio na hatia dhidi ya hatari kubwa na hofu ya kifo kutokana na machafuko na ukatili wote unaoendelea.”

Ziara ya Bwana O’Brien inafanyika wakati taifa hilo likikabiliwa na changamoto ya kufikisha misaada ya dharura kwa jamii zilizoathiriwa na mzozo.