Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa maji watishia afya Syria

Ukosefu wa maji watishia afya Syria

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limesema watu nusu milioni wanaoishi mjini Aleppo, nchini Syria, wanakumbwa na ukosefu wa maji, huku joto likizidi na huduma za maji zikiwa zimeharibika kwa sababu ya mapigano.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, UNICEF imetangaza kuwa imeanza kupeleka lita milioni 2.5 kila siku kwa wakazi wa Aleppo, msaada huo ukiwezesha shirika hilo kuwapatia watu 200,000 lita 15 za maji kwa siku. Aidha UNICEF imechimba visima 50, ambavyo vinaweza kutoa lita milioni 16 za maji kila siku.

Kwa mujibu wa UNICEF, maji hayakupatikana kabisa kwa kipindi cha wiki tatu zilizopita, hali hiyo ikisababisha hatari za magonjwa mbalimbali kama vile ugonjwa wa kuhara, hasa kwa watoto.

Juliette Touma ni msemaji wa UNICEF.

(SAUTI JULETTE)

“Ripoti zinaonyesha kuwa huduma za maji zimesitishwa makusudi mjini Aleppo na hiyo imeathiri zaidi ya watu milioni moja mjini humo. Unaweza kufikiria matokeo yake, pamoja na hali ya joto sana.”