Baraza la Usalama lalaani shambulizi la Julai 20 Uturuki

Baraza la Usalama lalaani shambulizi la Julai 20 Uturuki

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wamelaani vikali shambulizi la kigaidi lililotekelezwa mnamo Julai 20 kwenye kwenye eneo liitwalo Suruc, nchini Uturuki. Shambulizi hilo liliwaua watu wapatao 31 na kuwajeruhi wengine 100.

Wajumbe hao wa Baraza la Usalama wamepeleka risala za rambirambi kwa familia za wahanga, na kuwapa pole wote waliojeruhiwa katika shambulizi hilo, na kwa watu na serikali ya Uturuki ambayo ilipoteza raia wake.

Wamewatakia nafuu haraka waliojeruhiwa, na kusisitiza haja ya kuwakabili kwa mkono wa sheria watekelezaji wa vitendo vya kigaidi kama hivyo.

Wamekariri haja ya kupambana na tishio linaloletwa na vitendo vya kigaidi dhidi ya amani na usalama wa kimataifa kwa njia zote, kulingana na Katiba ya Umoja wa Mataifa, wakiongeza kuwa vitendo vyovyote vya kigaidi ni uhalifu, bila kujali kichochezi, lini vinafanyika, wapi vinakofanyika au nani anayevifanya.