Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wahofia hatma ya raia katika mji wa Zabadani, Syria

UM wahofia hatma ya raia katika mji wa Zabadani, Syria

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura, ameelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya raia katika mji wa Zabadani nchini Syria.

Vyombo vya habari na duru nyingine ndani ya mji huo zimeripoti mashambulizi makali ya bomu tangu vikosi vya serikali na wanamgambo wanaovounga mkono walipoanza kampeni dhidi ya wapiganaji wa upinzani walioko Zabadani.

Duru za kuaminika mashinani zimethibitisha kuwa idadi kubwa ya mabomu yamerushwa kwenye mji huo na kusababisha uharibifu ambao haujawahi kushuhudiwa, pamoja na vifo vya raia wengi.

Vikosi vya upinzani vilivyojihami viitwavyo ‘Jeshi la Ushindi’ vimejibu kwa kurusha mizinga na makombora kwenye vijiji viwili vya Al Foua na Kefraya karibu na mji wa Idlib, ambako idadi kubwa ya raia wamenaswa.

Bwana de Mistura ametoa wito kwa pande zote kuheshimu kanuni za ulinzi wa raia, na kwa serikali ya Syria kusitisha matumizi ya silaha mbovu na ambazo hazilengi shabaha, kama mabomu dhidi ya miji yake.