Hakuna watoto tena kwenye jeshi la DRC: MONUSCO
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, MONUSCO, umesema kuwa hakuna mtoto hata mmoja aliyesajiliwa kwenye jeshi la kitaifa la DRC, FARDC tangu mwanzo wa mwaka huu.
Hii ni kwa mujibu wa idara ya ulinzi wa watoto wa MONUSCO iliyotangaza takwimu hizo wakati wa kuadhimisha miaka kumi ya azimio nambari 1612 la Baraza la Usalama kuhusu watoto vitani, ikisema FARDC wamejitahidi kukijizuia kabisa kutumikisha watoto.
MONUSCO imeipongeza serikali ya DRC kwa jitihada zake katika kusalimisha watoto waliotumikishwa jeshini. Idadi ya watoto waliotumikishwa na FARDC imepungua kutoka 842 mwaka 2009 hadi sifuri mwaka huu.