Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Meli ya kwanza ya WFP yafika Aden kupeleka chakula

Meli ya kwanza ya WFP yafika Aden kupeleka chakula

Meli ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP iliyobeba tani 3,000 za chakula imewasili leo kwenye bandari ya Aden nchini Yemen, ikiwa ni mara ya kwanza kwa meli ya WFP kufika kule tangu mwanzo wa mapigano mwezi Machi.

Kwenye taarifa yake, WFP imesema msaada huo utawezesha watu 180,000 kupata chakula kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Akihojiwa na redio ya Umoja wa Mataifa, msemaji wa WFP Reem Nada amesema hii ni hatua kubwa katika jitihada za WFP za kufikisha misaada ya kibinadamu.

(SAUTI NADA)

“Ingawa tulikiwa tunaweza kufikia ukanda wa kusini kupitia mitandao ya barabara, ilikuwa muhimu sana kufikia ukanda wa kusini moja kwa moja kupitia bandari, kwa sababu inaharakisha operesheni zetu, tunaweza kufikia watu wengi zaidi kwa njia hiyo kwenye ukanda wa kusini hasa.”

WFP ilikuwa imejaribu mara nyingi kufikisha misaada kwa njia ya meli lakini haikuwezekana kuwasili bandarini kwa sababu ya mapigano. WFP imesema meli nyingine zinasubiri bado baharini mbele ya bandari.

Bi Nada ameongeza kuwa chakula kimetoweka kabisa kwenye masoko na maduka ya ukanda wa kusini, akieleza kuwa maduka ya mkate yamefungwa kwa kuwa hakuna hata mafuta ya kusagisha unga wa ngano. Kwa mujibu wa WFP, zaidi ya watu milioni 6 wanahitaji msaada wa chakula ili waokoe maisha yao.