Skip to main content

Mkuu wa OCHA O’Brien kuzuru Sudan Kusini

Mkuu wa OCHA O’Brien kuzuru Sudan Kusini

Mkuu wa masuala ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa Stephen O’Brien, anatarajiwa kuwasili nchini Sudan Kusini hapo kesho Jumatano kuanza ziara ya siku nne, ili kujionea moja kwa moja athari za kibinadamu za mzozo ambao umekuwa ukiendelea nchini humo, pamoja na jitihada za mashirika ya kutoa misaada katika kukabiliana na mahitaji ya kibinadamu yanayoongezeka.

Zaidi ya watu milioni 2.2 wamelazimika kuhama makwao Sudan Kusini, wakiwemo milioni 1.6 ambao ni wakimbizi wa ndani na 600, 000 waliokimbilia nchi za Sudan, Ethiopia, Kenya na Uganda.

Wakati wa ziara yake, Bwana O’Brien anatarajiwa kukutana na jamii za waathirika wa machafuko, maafisa wa ngazi ya juu serikalini, wadau wa kibinadamu na wanadiplomasia ili kujadili kuhusu mzozo huo na njia za kuimarisha operesheni za kibinadamu.

Wakati akijiandaa kwa ziara hiyo, Shirika la Afya Duniani, WHO limesema kuwa kufikia sasa, vimeripotiwa visa zaidi ya 1,210 vya kipindupindu nchini humo, vikiwemo vifo 39 katika kata za Juba na Bor, huku juhudi za kupambana na mlipuko huo zikishika kasi.