Mkakati wa Sendai kuhusu majanga wang’oa nanga

Mkakati wa Sendai kuhusu majanga wang’oa nanga

Juhudi za kimataifa za kutekeleza mkakati wa Sendai kuhusu kupunguza hatari za majanga zimeanza leo, huku nchi za bara Afrika zikiongoza juhudi hizo.

Juhudi hizo zimeanza kwa mkutano wa nchi arobaini na nane za Afrika mjini Yaoundé, Cameroon, kwa mazungumzo ya siku tatu ambayo pia yanajumuisha Muungano wa Afrika, AU, jumuiya za kikanda na mashirikia mengine ya kimataifa.

Lengo la mkutano huo ni kuoanisha mikakati iliyopo barani Afrika ya kupunguza hatari za majanga na mkakati wa Sendai, ambao ulipitishwa mnamo mwezi Machi mjini Sendai, Japan, ukilenga kuchukua hatua za kupunguza hatari za majanga kati ya mwaka 2015 na 2030.

Olushola Olayide, ambaye ni Mkuu wa idara ta mazingira, tabianchi, maji na udhibiti wa ardhi katika AU, amesema ni wakati wa kuweka barabara ya kutekeleza mkakati wa Sendai kikamilifu, kwani hiyo ndiyo njia pekee ya bara Afrika kuzuia hatari za majanga na madhara husika, ambayo yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 700,000 na hasara ya dola bilioni 1.3 za kiuchumi katika kipindi cha muongo mmoja.