Raia zaidi wa Nigeria wakimbilia Cameroon: UNHCR

Raia zaidi wa Nigeria wakimbilia Cameroon: UNHCR

Majuma kadhaa baada ya uchaguzi nchini Nigeria, machafuko na mashambulizi bado yanashika kasi nchini humo na kuathiri raia, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR. UNHCR imesema raia hao wanamiminika kwa wingi kaskazini mwa nchi jirani ya Cameroon wakikimbia eneo la mpakani kati ya nchi hizo ambalo linaelezwa kuwa na machafuko.

Wafanyakazi wa UNHCR walioko katika eneo hilo wanasema familia kadhaa zinawasili kwa wastani wa watu 100 kwa siku ambao wanajisajili  katika kambi iliyofunguliwa mwaka 2013. Idadi ya wakimbizi kambini hapo sasa imeongezeka kutoka 30,000 mwaka jana hadi 44,000 hivi sasa.

Leo Dobbs ni afisa wa UNHCR

"Wengi wanaowasili ni kutoka Nigeria na wanasema wamekimbia Borno kwa ajili ya mashambulio. Waliwasili mapema lakini wamepiga kambi karibu na mipaka kwa sababu walitarajia kurejea nyumbani haraka, UNHCR na serikali wamekuwa wakiwaomba waende kusini, eneo la Minawau ambako watakuwa na usalama zaidi na ambako wataweza kusaidiwa."