Skip to main content

Ban Ki-moon aeleza wasiwasi wake kuhusu uchaguzi Burundi

Ban Ki-moon aeleza wasiwasi wake kuhusu uchaguzi Burundi

Leo uchaguzi wa rais ukifanyika nchini Burundi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameziomba mamlaka za serikali kuhakikisha usalama na amani wakati wa uchaguzi huo.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake, Bwana Ban ameeleza wasiwasi wake baada ya mazungumzo ya kisiasa kusimamishwa mnamo tarehe 14, Julai bila kufikia makubaliano.

Hata hivyo amepongeza jitihada za rais wa Uganda Yoweri Museveni na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika kuhamasisha mazungumzo hayo.

Katibu Mkuu amekariri wito wake wa kuanzisha tena mazungumzo baina ya pande zote za kisiasa nchini Burundi, akiwasihi kujizuia na vitendo vya ghasia vinavyoweza kuharibu mafanikio ya mwafaka wa Arusha katika kujenga demokrasia.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kufuatilia uchaguzi nchini Burundi, MENUB, unaendelea kutekeleza wajibu wake na umeshasambaza waangalizi nchini kote ili kutimiza majukumu hayo.