Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bei ya vipimo vya Ukimwi yapungua: UNAIDS

Bei ya vipimo vya Ukimwi yapungua: UNAIDS

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya HIV na ukimwi, UNAIDS, limetangaza kuunda makubaliano mapya na shirika la madawa la kiswisi Roche Diagnostics ili kupunguza kwa asilimia 35 bei ya vipimo vya ukimwi kwa watoto wachanga.

Kwenye taarifa iliyotolewa jumapili, UNAIDS imekaribisha ushirikiano huo ikisema sasa bei ya kipimo kimoja itakuwa ni dola 9.40.

UNAIDS imeeleza kuwa ni nusu tu ya watoto wachanga waliokuwa na hatari ya kuambukiwzwa na ukimwi ndio wanaopimwa mapema kwa sababu bei kubwa ya vipimo inawazuia wengi kupata huduma hiyo kwenye nchi zinazoendelea. Aidha ni asilimia 32% tu ya watoto wanaoishi na virusi vya ukimwi ndio wanapewa matibabu, ikiwa ni asilimia 41% kwa watu wazima.

Mkurugenzi mtendaji wa UNAIDS Michel Sidibé amesema makubaliano hayo na Roche Diagnostics ni hatua muhimu katika kufikia lengo la kuwezesha asilimia 90 ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi kujua hali yao na kuwapatia matibabu.