Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 19.3 wamefurushwa makwao kutokana na majanga: Ripoti

Watu milioni 19.3 wamefurushwa makwao kutokana na majanga: Ripoti

Mtu mmoja amekuwa akilazimika kuhama anakoishi kila sekunde kwa sababu ya janga kwa kipindi cha miaka saba iliyopita, huku watu milioni 19.3 wakilazimika kukimbia makwao mwaka 2014 pekee. Takwimu hizo ni kutokana na ripoti ya pamoja ya kitengo cha kufuatilia uahmiaji wa lazima(IDMC) na Shirika la Norwegian Refugee Council (NRC) iliyotolewa Jumatatu .

Ripoti hiyo iitwayo makadirio ya kimatifa: Watu waliofurushwa na majanga inaelezea jinsi watu milioni 17.5 mwaka 2014 walilazimika kukimbia makwao kufuatia majanga yatokanayo na hali ya hewa ikiwemo, mafuriko na dhoruba na watu milioni 1.7 wakifurushwa na sababu zitokanazo na matetemeko ya ardhi.

Kadhalika ripoti hiyo imetaja bara Asia kama eneo lililoathirika pakubwa na majanga huku bara hilo likitajwa kama eneo lililo hatarini zaidi kwa majanga. William Lacy Swing ni mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM, ambaye alishiriki utafiti huo.

“Changamoto ambayo ripoti hii inaangazia ni kuhakikisha kwamba wale walio hatarini zaidi baada ya janga hawasahauliki kwa sababu mara nyingi huenda wakasahaulika baada ya janga , na utoaji wa msaada kuna hatari ya wao kusahaulika”

Bwana Swing ameongeza kwamba wakati mizozo ikiendelea nchini Somalia, Yemen na Syria na changamoto za Boko Harama zikishuhudiwa kuna hatari ya kusahaulika kwa waathirika wa majanga ya asili.