Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafua ya ndege yatishia Afrika Magharibi

Mafua ya ndege yatishia Afrika Magharibi

Shirika la Kilimo na Chakula FAO limesema dola milioni 20 zinahitajika ili kusitisha mlipuko wa mafua ya ndege aina ya H5N1 kwenye ukanda wa Afrika magharibi.

Wito huo umetolewa leo kufuatia mlipuko wa ugonjwa huo kwenye viwanda vya kuku, masoko na nyumba za familia nchini Nigeria, Burkina Faso, Niger, Cote d’Ivoire na Ghana, huku FAO ikihofia maambukizi yanaweza kuenea kwenye ukanda mzima na hata zaidi, mlipuko huo usipodhibitiwa.

Daktari Juan Lubroth, Daktari mkuu wa mifugo wa FAO, amesema bado vifo vya binadamu havijatokea lakini ni muhimu kuzuia usambazaji wa ugonjwa huo.

“ Nasisistiza umuhimu wa kukabiliana na tatizo hilo kwenye sekta ya ufugaji wa kuku kabla mlipuko huo usambazwe kwenye jamii nyingine, viwanda vya kuku vingine au nchi zingine. Ushirikiano na wizara ya afya ni muhimu sana ili kuweza kuelimisha jamii kabla mlipuko uenee.”

Kwa mujibu wa FAO, mafua ya ndege yanaweza kusababisha vifo vya mamilioni ya kuku na hivyo kuathiri ukuaji wa uchumi.

Milipuko mingine imetokea barani Asia na Misri tangu mwaka 2000, ikiathiri pia afya na uhai wa binadamu.