Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yapongeza ujenzi mpya wa makumbusho mjiniTimbuktu Mali

UNESCO yapongeza ujenzi mpya wa makumbusho mjiniTimbuktu Mali

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO limepongeza hatua ya ujenzi mpya wa makumbusho ya mjini Timbuktu nchini Mali miaka mitatu baada ya kuharibiwa na vikundi vyenye silaha.Taarifa kamili na Joseph Msami.

(TAARIFA YA MSAMI)

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Irina Bokova ambaye amefanya ziara katika makumbusho hayo hapo jana amepongeza jamii ya Timbuktu akisema bila ridhaa yao ujenzi huo usingefanyika.

Ziara hiyo iliwaleta pamoja viongozi wa serikali na dini akiwamo waziri wa utamaduni, Sanaa na utalii , waziri wa elimu pamoja na mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Mali Mongi Hamdi pamoja na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya .

Bi Bokova amesema wenyeji na waashi wa Timbuktu ambao hamasa na ujuzi wao umetoa mchango mkubwa katika ujenzi wa makumbusho hayo muhimu kwa historia ya Mali, pia ni somo la stahamala, majadiliano na amani.

Mkuu huyo wa UNESCO alikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa hilo ni somo na jawabu kwa vikundi vyote vyenye msimamo mikali ambavyo mwangwi wao waweza kusikika nje ya mipaka ya Mali.