Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laidhinisha makubaliano ya nyuklia baina ya Iran na P5+1

Baraza la Usalama laidhinisha makubaliano ya nyuklia baina ya Iran na P5+1

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limeidhinisha makubaliano ya mpango wa pamoja wa kuchukua hatua kuhusu mpango wa nishati ya nyuklia nchini Iran, JCPOA. Taarifa kamili na Grace Kaneiya

(Taarifa ya Grace)

Makubaliano hayo yalifikiwa wiki iliyopita baina ya Iran na wanachama wa kudumu wa Baraza hilo, pamoja na Ujerumani na Muungano wa Ulaya, EU, Iran ikiahidi kuwa kamwe haitajaribu kuunda au kupata silaha za nyuklia kwa namna yoyote ile.

Wajumbe wa Baraza la Usalama wamesisitiza umuhimu wa juhudi za kisiasa na kidiplomasia katika kupata suluhu la mazungumzo, ambalo linahakikisha kuwa mpango wa nishati ya nyuklia nchini Iran ni kwa minajili ya amani tu.

Kwa mantiki hiyo, wajumbe wa Baraza la Usalama wameidhinisha makubaliano hayo na kutoa wito yatekelezwe kikamilifu, kulingana na ratiba iliyowekwa katika JCPOA.

Wametoa wito pia kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki, IAEA aanze kuhakiki na kufuatilia utekelezaji wa ahadi ilizotoa Iran kuhusu nyuklia, kama msingi wa kuondoa baadhi ya vikwazo ilivyowekewa.