Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi zinazotimiza lengo utoaji chanjo zimeongezeka maradufu-WHO

Nchi zinazotimiza lengo utoaji chanjo zimeongezeka maradufu-WHO

Idadi ya nchi zinazotimiza na kuendeleza lengo la kutoa chanjo za kuokoa maisha kwa asilimia 90 ya watoto, imeongezeka maradufu tangu mwaka 2000, limesema Shirika la Afya Duniani, WHO.

Takwimu za hivi karibuni kuhusu mwelekeo wa utoaji chanjo duniani zimebainisha kuwa, mnamo mwaka 2014, nchi 129, zikiwa ni sita zaidi tangu mwaka 2013, sasa zinatoa chanjo kwa angalau asilimia 90 ya watoto dhidi ya magonjwa ya diphtheria, pepo punda na pertussis (DTP3).

Mnamo mwaka 2012, nchi zote 194 wanachama wa WHO ziliuridhia mkakati wa kimataifa wa kuchukua hatua za utoaji chanjo (GVAP), na kuahidi kuhakikisha kuwa hakuna mtu hata mmoja anayekosa kupatiwa chanjo muhimu, zikilenga kutimiza asilimia 90 ya utoaji chanjo ya DTP3 katika nchi zote ifikapo mwaka 2015.

Takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa nchi 65 zitahitaji kuweka mikakati inayobadilisha hali, ili kutimiza lengo la mkakati wa kimataifa wa utoaji chanjo, zikiwemo nchi 6 ambazo zinatoa chanjo ya DTP3 kwa chini ya asilimia 50 ya watoto. Nchi hizo sita ni Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Equatorial Guinea, Somalia, Sudan Kusini na Syria.