Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalam wa UM walitaka Baraza la Usalama lichukue hatua kuzuia machafuko Burundi

Wataalam wa UM walitaka Baraza la Usalama lichukue hatua kuzuia machafuko Burundi

Kundi la wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, leo wametoa wito kwa Baraza la Usalama lichukue hatua mara moja kuzuia Burundi kutumbukia tena katika machafuko, kabla ya uchaguzi wa urais.

Wataalam hao wa haki za binadamu wamesema iwapo Burundi itatumbukia katika machafuko zaidi, mzozo huo utaathiri nchi nyingine katika ukanda wa Maziwa Makuu, zikiwemo Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Tayari watu 145,000 wamekimbilia nchi jirani wakihofia uhai wao kutokana na machafuko nchini Burundi.

Wataalam hao wamesema dunia inashuhudia kuongezeka kwa ghasia zinazochochewa na siasa nchini Burundi, zikiwezeshwa pia na miongo mingi ya ukwepaji sheria nchini humo. Wameongeza kuwa jamii ya kimataifa isisubiri hadi mauaji ya halaiki yaibuke na hatari ya mzozo kuathiri ukanda mzima ndipo ichukue hatua.