Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zifanyeni ahadi za kuwekeza katika watoto ziwe vitendo- UNICEF

Zifanyeni ahadi za kuwekeza katika watoto ziwe vitendo- UNICEF

Shirika la Kuhudumia Watoto UNICEF, limetoa wito kwa viongozi wanaoshiriki kongamano la kimataifa kuhusu ufadhili kwa maendeleo wazifanye ahadi zao za kuwekeza katika watoto na vijana kuwa vitendo, ili kupunguza tofauti za kitabaka na kumpta kila mtoto fursa nzuri katika maisha.

UNICEF imekaribisha utambuzi wa kongamano hilo linalomalizika leo mjini Addis Ababa kuwa kuwekeza katika watoto na vijana ni muhimu katika kufikia maendeleo jumuishi, yenye usawa na endelevu.

Shirika hilo limesema hii inaonyesha kubadili dhana kuwa watoto ni watu wanaonufaika tu kutokana na uwekezaji wa kijamii, na kuwaona kama kichochezi cha ukuaji na maendeleo katika siku za usoni.

UNICEF pia imeunga mkono utambuzi wa kongamano hilo kuwa ni muhimu kuendeleza na kulinda haki za watoto wote, na kuhakikisha kuwa hakuna mtoto anayeachwa nyuma.

Hivyo, UNICEF imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kufanya kipaumbele uwekezaji katika huduma za msingi kama elimu, mitandao ya usalama wa kijamii, afya, chanjo, maji na kujisafi, na ulinzi wa watoto.