Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi za Afrika zapaswa kuongeza ushuru ili kufadhili maendeleo yao: IMF

Nchi za Afrika zapaswa kuongeza ushuru ili kufadhili maendeleo yao: IMF

Mfuko wa fedha wa kimataifa IMF utaongeza kwa asilimia 50 upatikanaji wa mikopo kwa nchi zenye kipato cha chini, na pia kusaidia nchi zinazoendelea kuimarisha mifumo yao ya ushuru. Maamuzi hayo mawili yametangazwa wiki hii kwenye kongamano la kimataifa kuhusu ufadhili wa maendeleo linaloendelea mjini Addis Ababa, Ethiopia. Taarifa kamili na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Akizungumza na idhaa hii, Naibu Mkurugenzi wa IMF kuhusu masuala ya sera, mikakati na tathmini, Sean Nolan, amesema nchi 70 zenye kipato cha chini zitafaidika na upatikanaji mkubwa zaidi wa mikopo isiyokuwa na riba, akieleza kwamba IMF sasa inajitahidi kufuatilia uendelevu wa madeni ya nchi hizo.

Halikadhalika, IMF na Benki ya Dunia zimezindua mkakati mpya wa kusaidia nchi zinazoendelea kuimarisha ukusanyaji wa ushuru, ambao Bwana Nolan ameutaja kama msingi wa kujenga taifa na kujitegemea kiuchumi.

Nchi ambayo inataka kukuza maendelo kupitia miundombinu, afya na elimu inapaswa kukusanya yenyewe pesa hizo. Kiwango cha ushuru ni kidogo sana kwenye nchi nyingi barani Afrika, na kinaweza kuongezwa kirahisi. Kuongeza kipato cha kitaifa haimaanishi kuwatoza watu waliopo shambani ushuru mkubwa. Inamaanisha kuwatoza ushuru watu tajiri na makampuni ya kitaifa na kimataifa kwa njia bora zaidi.”

Pamoja na makubaliano ya kimataifa kuhusu ufadhili kwa maendeleo yaliyopatikana alhalmis usiku, nchi wanachama na mashirika ya kimataifa yamejituma nchini Ethiopia kukuza maendeleo endelevu kupitia mikakati thabiti.