Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Twahitaji ufadhili na kuwezeshwa kuwafikia wahitaji hima Yemen - OCHA

Twahitaji ufadhili na kuwezeshwa kuwafikia wahitaji hima Yemen - OCHA

Mashirika ya kibinadamu nchini Yemen yametoa wito wa ufadhili na kuwezeshwa kuwafikia wahitaji  kwa dharura.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Kuratibu masuala ya Kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, OCHA, mashirika hayo yametoa wito kwa pande kinzani katika mzozo wa Yemen kuwalinda raia kulingana na sheria ya kimataifa ya kibinadamu, pamoja na kuwezesha wahudumu wa kibinadamu kufikisha usaidizi kwa watu wanaouhitaji.

Taarifa imesema, raia wa Yemen wameendelea kuteseka wakati machafuko yakiongezeka bila kuonyesha dalili ya kusitishwa, wiki hii ikiwa imeshuhudia maafa makubwa zaidi tangu mwezi Machi.

Takriban watu milioni 1.3 wamelazimika kuhama makwao kwa sababu za kiusalama, huku watu wanaohitaji misaada ya kibinadamu, wakiwa ni milioni 21, ambayo ni sawa na asilimia 80 ya idadi nzima ya watu Yemen. Kufikia sasa, watu zaidi ya 3,500 wameuawa, na wengine 16,000 kujeruhiwa.

Mahitaji ya kibinadamu yamezidi uwezo wa kutoa usaidizi, huku ombi la ufadhili likiwa limepokea asilimia 15 tu ya dola bilioni 1.6 zinazohitajika hadi mwishoni mwa mwaka huu 2015.