Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali nchini Libya bado ni tete, mazungumzo ya kisiasa yahitajika- Leon

Hali nchini Libya bado ni tete, mazungumzo ya kisiasa yahitajika- Leon

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa ujumbe wa usaidizi wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, UNSMIL, Bernardino Leon, ameliambia Baraza la Usalama leo kuwa licha ya kuanza makubaliano ya kisiasa kuhusu mkakati wa mazungumzo zaidi ya amani, hali nchini Libya imeendelea kuzorota kutokana na migawanyo ya kisiasa na machafuko.

Ameongeza kwamba watu wengi wameendelea kuuawa, huku kukiendelea kuwepo uharibifu mkubwa.

Bwana Leon amesema kutokuwepo usalama kunazuia kuanza tena kwa kazi ya vyombo vya sheria Benghazi, Derna na Sirte, huku mjini Tripoli, mara ya mwisho kusikikilizwa kesi dhidi ya Saif al-Islam Qadhafi, Abdullah al-Senussi, na maafisa wengine 35 wa serikali ya Gaddafi kwa uhalifu uliotedwa wakati wa mzozo wa 2011 kukiwa kulifanyika mnamo tarehe 20 Mei, huku hukumu ikitarajiwa kufanywa mnamo Julai 28.

Libya ni lazima ikabiliane na ukurasa huu wenye doa katika historia yake, kwa kuwawajibisha waliotenda uhalifu mbaya sana kisheria, kulingana na viwango vya kimataifa vya sheria na haki."

Aidha, Bwana Leon ameeleza kutiwa wasiwasi na hali ya kibinadamu nchini Libya

Hali ya kibinadamu kwa ujumla inaendelea kutia wasiwasi, idadi ya wakimbizi wa ndani ikiwa imeongezeka maradufu tangu Septemba mwaka uliopita, na ufadhili haba kwa jitihada za kibinadamu. Awbari, Ghat na maeneo mengine Kusini yanayohitaji misaada, bado hayawezi kufikiwa na mashirika ya kimataifa ya kibinadamu kwa sababu ya kuzorota kwa hali ya usalama.”

Bwana Leon amesema Libya ipo katika hali tete, akiomba Baraza la Usalama litoe wito kwa pande kinzani nchini Libya kuendelea kushiriki katika mchakato wa mazungumzo, akisema kwamba ni kupitia katika mazungumzo ya kisiasa tu ndipo suluhu la amani litapatikana kwa mzozo huo.