Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubia wa kimataifa wazinduliwa kutokomeza ukatili dhidi ya watoto

Ubia wa kimataifa wazinduliwa kutokomeza ukatili dhidi ya watoto

Ubia mpya wa kimataifa umezinduliwa na Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Ukatili dhidi ya Watoto, Santos Pais, na wadau wengine ukilenga kutokomeza ukatili dhidi ya watoto.

Mkakati huo uliozinduliwa mjini Addis Ababa wakati wa kongamano la tatu kuhusu Ufadhili kwa Maendeleo, unalenga kuchagiza rasilmali na kutekeleza lengo namba 16.2 la malengo ya maendeleo endelevu (SDGs), ambalo ni kutokomeza dhuluma, unyanyasaji, usafirishaji haramu na aina zote za ukatili na utesaji dhidi ya watoto.

Ubia huo unatarajiwa kuchagiza uungwaji mkono katika kanda tofauti, ili kutekeleza lengo hilo la maendeleo endelevu, na pia kuwa chagizo la uwekezaji zaidi katika vyombo vya kupunguza ukatili dhidi ya watoto, pamoja na kuchagiza ufadhili zaidi.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Santos Pais amesema ubia huo mpya na mfuko wa kutokomeza ukatili dhidi ya watoto utakuwa sehemu muhimu katika utekelezaji wa SDGs.