Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban apongeza makubaliano kuhusu nyuklia kati ya P5+1 na Iran

Ban apongeza makubaliano kuhusu nyuklia kati ya P5+1 na Iran

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amepongeza makubaliano kuhusu nyuklia yaliyosainiwa baina ya Iran kwa upande mmoja, na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama, zikiwa ni Marekani, Uchina, Ufaransa, Uingereza  na Urusi, pamoja na Ujerumani, akiyataja kama ya kihistoria.

Ban ametaja makubaliano hayo kama ishara ya thamani ya mazungumzo, akipongeza ari na juhudi za washiriki, pamoja na ujasiri wa viongozi walioidhinisha makubaliano hayo yaliyofikiwa mjini Vienna, Austria.

“Natumai, na kuamini kuwa makubaliano haya yatachangia uelewano zaidi na ushirikiano kuhusu changamoto nyingi sugu za kiusalama Mashariki ya Kati. Kwa hiyo, yanaweza kuwa mchango muhimu kwa amani na ustawi katika ukanda huo na kwingineko.”

Ban amesema Umoja wa Mataifa u tayari kushirikiana kikamilifu na pande zote katika makubaliano hayo katika harakati za kuyatekeleza.