Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubia utaendeleza ukuaji wa sekta ya viwanda- UNIDO

Ubia utaendeleza ukuaji wa sekta ya viwanda- UNIDO

Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda UNIDO limetoa wito kwa ushirikiano wa wadau ili kukuza sekta ya viwanda kwa njia endelevu. Taarifa kamili na Priscilla Lecomte.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNIDO Li yong amesema hayo katika mkutano maalum kuhusu maendeleo jumuishi na endelevu ya viwanda, wakati wa kongamano la tatu la kimataifa kuhusu ufadhili kwa maendeleo, linalofanyika mjini Addis Ababa. Ameeleza kwamba hakuna maendeleo na ukuaji wa uchumi bila kuwekeza katika sekta ya viwanda.

Kwa mtazamo wangu, changamoto hii ni kubwa mno kiasi kwamba nchi au serikali moja haiwezi kukabiliana nayo pekee yake. Naamini kwamba changamoto hii inaweza kukabiliwa tu kupitia ubia unaoshirikisha wadau wote katika harakati za maendeleo.”

Mkuu wa UNIDO ameipongeza Ethiopia kwa mafanikio yake kupitia mkakati mpya ulioanzisha na UNIDO. Ukuaji wa uchumi nchini Ethiopia umefika zaidi ya asilimia kumi kwa mwaka kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema maendeleo ya viwanda ni moja ya malengo ya maendeleo endelevu yatakayoamuliwa mwezi Septemba mwaka huu, akisisitiza umuhimu wa kukuza sekta ya viwanda kwa njia endelevu na jumuishi ili kutunza mazingira na kuzalisha ajira bora.