Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNAMA alaani shambulizi la bomu Khost, Afghanistan

Mkuu wa UNAMA alaani shambulizi la bomu Khost, Afghanistan

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Afghanistan, Nicholas Haysom, amelaani vikali shambulio la hapo jana la kujitoa mhanga katika mji wa Matun, mkoa wa Khost nchini Afghanistan, ambalo liliwaua raia 27 na kuwajeruhi wengine 10.

Miongoni mwa waliouawa ni wanawake watatu, na watoto 12. Shambulizi hilo pia liliwaua maafisa sita wa vikosi vya usalama wa Afghanistan.

Shambulizi hilo lilifanyika hapo jana jioni muda mfupi kabla ya watu kufuturu, pale mlipuaji huyo wa kujitoa mhanga alipoegesha gari lililojaa vilipuzi karibu na eneo la upekuzi wa usalama karibu na soko la jamii.

Bwana Haysom amesema shambulizi kama hilo haliwezi kukubaliwa, na kwamba waliopanga shambulizi hilo wanapaswa kuwajibishwa kisheria.