Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutojiandaa vyema kwa majanga kunakwamisha maendeleo- Wahlstrom

Kutojiandaa vyema kwa majanga kunakwamisha maendeleo- Wahlstrom

Kutojiandaa vyema na kushindwa kutoa kinga dhidi ya majanga kunakwamisha maendeleo ya kimataifa, amesema Mkuu wa Shirika la kuchukua tahadhari na kupunguza athari za majanga, Margareta Wahlstrom.

Bi Wahlstrom amesema hayo mjini Geneva kabla ya kuelekea Addis Ababa kwa kongamano la tatu la ufadhili kwa maendeleo, akiwa na ujumbe kuwa nchi nyingi zaidi zinapaswa kufanya mipango ya kukabiliana na majanga kuwa sehemu muhimu ya mipango yao ya maendeleo.

Katika mahojiano na Radio ya Umoja wa Mataifa, Bi Wahlstrom amesema nchi nyingi sana hutegemea hatua za dharura kukabiliana na matatizo, na mitazamo ya muda mfupi ambayo mara nyingi inaziacha zikiwa dhoofu zaidi kuliko zainavyotakiwa kuwa, kila janga linapoibuka.

Ukitizama ukubwa wa tatizo hili, hatujaweza kupunguza idadi ya maangamizi bado. Katika baadhi ya maeneo duniani, nchi zimefanikiwa sana, lakini kwa ujumla, kiwango cha maangamizi katika majanga kinaendelea kupanda. Tumejikita kwa kutafuta suluhu ya dharura kwa muda mfupi. Tumeacha desturi ya kupanga na kujiandaa kwa muda mrefu na kuandama ile ya suluhu ya muda mfupi, kutotaka kuwekeza katika kujiandaa, kwani hakuna faida ya papo hapo.”