Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ahadi ni deni: Ban Ki-moon atoa wito kwa ufadhili wa maendeleo

Ahadi ni deni: Ban Ki-moon atoa wito kwa ufadhili wa maendeleo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema mwaka 2015 utakuwa mwaka wa kuchukua hatua, ili ahadi za ufadhili wa maendeleo zitimizwe. Taarifa kamili na Amina Hassan.

Taarifa ya Amina

Ban amesema hayo akizindua kongamano la tatu la kimataifa kuhusu Ufadhili kwa Maendeleo, FFD, mjini Addis-Ababa, Ethiopia.

Katibu Mkuu amesema mfumo mpya wa maendeleo utakaokubaliwa na nchi wanachama utahakikisha hakuna mtu atakayeachwa nyuma.

“ Katika dunia ya leo, ambako idadi ya watu inaongezeka, na halikadhalika mahitaji ya fedha, ufadhili kwa maendeleo unapaswa kuanzishwa upya. Suluhu ni kutumia vyanzo vyote vya ufadhili: kutoka serikali, sekta binafsi, ndani ya nchi na kimataifa. Hii ni pamoja na sera imara na mifumo ya udhibiti wa uchumi, na vichochezi vya mabadiliko katika matumizi na uzalishaji.”

Bwana Ban ameziomba nchi wanachama ziweze kufikia makubaliano, huku mazungumzo yakiendelea kuhusu azimio linalotarajia kupitishwa kabla ya mwisho wa kongamano hilo ili kuhakikisha ufadhili kwa ajili ya ajenda ya maendeleo ya baada ya mwaka 2015.