UM wasikitishwa na kutojumuishwa kwa wakimbizi katika uchaguzi CAR

UM wasikitishwa na kutojumuishwa kwa wakimbizi katika uchaguzi CAR

Mratibu wa masuala ya kibinadamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR,  Aurélien A. Agbénonci, ameeleza kusikitishwa na uamuzi wa Baraza la Kitaifa la Mpito kukataa wakimbizi wa CAR wasipige kura katika uchaguzi ujao wa urais.

Wengine walioelezea masikitiko kama hayo ni Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR na mashirika yote ya kibinadamu nchini CAR.

Wameeleza pia kuhofia athari za uamuzi huo katika juhudi za kuchagiza maridhiano na uiano wa kijamii katika nchi hiyo, huku Bwana Agbénonci akisema kuwa kutowajumuisha wakimbizi pia kutaathiri Imani katika uchaguzi huo, na kwamba uchaguzi unapaswa uwe huru, wa wazi na kumjumuisha kila mtu.

Tangu mwezi Disemba 2013, takriban asilimia 25 ya raia wa CAR wamelazimika kuhama makwao ndani ya nchi, huku wengine zaidi ya 460,000 wakiwa wamekimbilia nchi za Cameroon, Congo (Brazzaville), DRC na Chad.