Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika yasiyo ya kiserikali yana mchango mkubwa katika maendeleo:Ban

Mashirika yasiyo ya kiserikali yana mchango mkubwa katika maendeleo:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban-Ki-moon ameshukuru mashirika yasiyo ya kiserikali au CSO kwa utashi wao na uhamasishaji wao katika kushawishi nchi wanachama ili wawekeze zaidi katika kufadhili ajenda ya maendeleo endelevu.

Amesema hayo wakati wa hafla ya kufunga mkutano wa mashirika yasiyo ya kiserikali uliofanyika wikiendi hii kabla ya kongamano la tatu la kimataifa kuhusu ufadhili kwa maendeleo litakaloanza jumatatu hii mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Bwana Ban amesema mashirika ya kijamii yanajukumu la msingi katika kuwajibisha serikali ili kufadhili ajenda ya baada ya mwaka 2015.

Katibu Mkuu amemulika maeneo  ambapo jamii inaweza kuchangia pakubwa:

Kwanza, kukusanya kipato cha ndani. Ni muhimu sana, ajenda ya utekelezaji  imechukua hatua ndogo lakini muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kuhusu maswala ya ulipaji ushuru. Pili, nchi wafadhili zinapaswa kutimiza ahadi zao kuhusu msaada wa kitaifa wa maendeleo pamoja na ufadhili wa maswala ya tabianchi. Tatu, kiwango cha uwekezaji binafsi ni muhimu, lakini ubora wake pia;”

Bwana Ban amesema mashirika ya kijamii yanapaswa kushinikiza serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha uwekezaji endelevu.

Hatimaye amesema ni muhimu pia kuangazia mazingira ya ufadhili, kupitia maswala ya deni, biashara na utawala.

Kwa upande wao washiriki kutoka mashirika ya kijamii wamesisitiza umuhimu wa kuwekeza pesa zaidi katika maswala ya maendeleo na kuunda mfumo wa kimataifa wa kudhibiti ulipaji ushuru chini ya uongozi wa Umoja wa Mataifa.