Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanahabari Ethiopia wameachiwa lakini wengine bado kizuizini- Mtaalam

Wanahabari Ethiopia wameachiwa lakini wengine bado kizuizini- Mtaalam

Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa kujieleza, David Kaye, amekaribisha hatua ya kuachiwa huru hapo jana kwa mabloga wawili nchini Ethiopia, ambao walikuwa wakichangia kwa chapisho huru la ‘Zone 9’, pamoja na waandishi habari wengine wanne.

Hata hivyo, Bwana Kaye amesema waandishi wengine wa habari bado wapo kizuizini nchini humo, chini ya sheria dhidi ya ugaidi.

Amesema anatarajia kuwa hatua hiyo ni ya kwanza katika hatua nyingine kama hizo zitakazochukuliwa na mamlaka za Ethiopia kuwaachia huru waandishi wengine wa habari na wanaharakati waliowekwa rumande kwa kutenda kazi yao halali.

Mabloga hao ambao walikuwa wakitumia jukwaa la mtandao wa intaneti kuripoti kuhusu masuala ya kijamii na kisiasa nchini Ethiopia, walikamatwa mnamo mwaka 2014, na wamekuwa kizuizini kwa zaidi ya mwaka mmoja.