Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lasikitishwa na vitendo vya viongozi wa Sudan Kusini

Baraza la Usalama lasikitishwa na vitendo vya viongozi wa Sudan Kusini

Wajumbe wa Baraza la Usalama, wameelezea kusikitishwa mno na vitendo vya Rais Salva Kiir was Sudan Kusini, makamu wake wa zamani Riek Machar Teny, na viongozi wengine ambao wameweka maslahi yao binafsi mbele ya maslahi ya nchi na watu wao, na kuweka hatarini msingi wa taifa hilo change.

Wakitambua Julai 9 kama siku ya kuadhimisha mwaka wa nne wa uhuru wa Sudan Kusini wajumbe hao wa Baraza la Usalama wamesema kushindwa kwa viongozi hao wawili kuandama amani, kumesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya raia, kuwalazimu watu milioni 2.1 kuhama makwao, na kusababisha mashambulizi na mauaji ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa na wakimbizi wa ndani wanaopewa ulinzi na Umoja wa Mataifa, na wahudumu wa kibinadamu.

Wamelaani vikali ukiukaji wa haki za binadamu na ukiukaji wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu nchini humo, ukiwemo ule ulioripotiwa na UNICEF na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa, UNMISS katika majimbo ya Unity na Upper Nile mwezi Aprili na Mei 2015, ambo ulihusisha kuhasi, ubakaji wa halaiki na uteketezaji wa wanawake na watoto katika nyumba zao.

Wajumbe hao wa Baraza la Usalama wamesema kuwa vitendo kama hivyo haviweza kukubalika, huku wakieleza kusikitishwa na miezi 19 ya machafuko nchini Sudan Kusini, pamoja na janga la kisiasa, kiusalama, kibinadamu na kiuchumi linalosababishwa na mwanadamu.