Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNIDO na Benki ya EU kuchagiza maendeleo endelevu ya viwanda Afrika

UNIDO na Benki ya EU kuchagiza maendeleo endelevu ya viwanda Afrika

Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda, UNIDO, limekubaliana na Benki ya Ulaya ya Uwekezaji, EIB, kuchagiza maendeleo jumuishi na endelevu ya viwanda, hususan barani Afrika katika nchi za Ethiopia na Senegal ambako miradi ya UNIDO ya ubia inaendelea.

Halikadhalika, nchi zingine za kanda za Afrika, Karibi na Pasifiki zitamulikwa katika makubaliano hayo mapya, huku maeneo mengine kama vile Ulaya Mashariki, Mediterania, Asia ya Kati na Amerika Kusini yakilengwa pia.

Makubaliano hayo yaliyosainiwa nchini Luxembourg leo na Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO, Li Yong, na rais wa EIB, Werner Hoyer, yataangazia utoaji wa usaidizi katika shughuli za uwekezaji, kitaaluma na kutoa mafunzo kuhusu mbinu bora za uwekezaji kupitia mitandao ya UNIDO na EIB.Ushirikiano huo pia utawezesha na kuratibu operesheni, zikiwemo za ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, na kusaidia katika kuandaa, kutekeleza na kuratibu mikakati na miradi ya kuendeleza viwanda.