Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali Burundi yamulikwa katika Baraza la Usalama

Hali Burundi yamulikwa katika Baraza la Usalama

Hali nchini Burundi ni tete, na taifa hilo limo hatarini kutumbukia katika machafuko zaidi. Kauli hiyo imetolewa na Msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu masuala ya kisiasa Bwana Taye-Brook Zerihoun, wakati aklihutubia Baraza la Usalama.

Ametoa wito kwa serikali kutimiza wajibu wake wa kulinda raia wote wa Burundi na haki zao, na kwa upinzani kujiepusha na ghasia na kukubali kufanya mazungumzo ya kisiasa na serikali, akisema mazungumzo ndiyo njia pekee ya kutatua mzozo uliopo sasa na machafuko zaidi yanayotishia kulighubika taifa hilo..

Mwingine aliyeonya kuhusu uwezekano wa Burundi kutumbukia katika machfuko zaidi ni Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein, ambaye, kupitia njia ya video, ameliambia Baraza hilo kuwa kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Burudi..

Sauti ya Kamishna Zeid

"Waandamanaji wamewekwa rumande na kuteswa na kutendewa uovu mwingine. Tumepokea pia ripoti za mauaji kinyume na sheria, na hadi sasa, ukiukwaji huu haujachunguzwa au kukabiliwa kisheria."