Skip to main content

Wajawazito hatarini kufuatia vifo vya wahudumu wa afya kutokana na Ebola - ripoti

Wajawazito hatarini kufuatia vifo vya wahudumu wa afya kutokana na Ebola - ripoti

Wakati mashauriano yakiendelea hapa mjini New York kuhusu kongamano la ukwamuaji wa nchi za Afrika Magharibi kutokana na athari za Ebola, ripoti mpya ya Benki ya Dunia imesema kuwa kufariki dunia kwa wahudumu wengi wa afya kutokana na mlipuko wa Ebola huenda kukasababisha vifo vya wanawake 4,022 zaidi kila mwaka katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone, kutokana na matatizo ya mimba na kujifungua.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Benki ya Dunia inayohusu vifo vya wahudumu wa afya na Ebola, mlipuko wa Ebola Afrika Magharibi huenda ukaacha madhara makubwa zaidi kuliko yale ya moja kwa moja ya ugonjwa huo, mathalan vifo na ulemavu.

Mchumi mkuu wa Benki ya Dunia, Markus Goldstein, ambaye pia ni mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo, amesema vifo vya waja wazito kutokana na kupoteza wahudumu wengi wa afya huenda vikapanda hadi kufikia viwango ambavyo havijakuwepo tangu miaka 15-20 iliyopita.

Ripoti imesema vifo vya wajawazito huenda vikapanda kwa asilimia 38 nchini Guinea, asilimia 74 nchini Sierra Leone, na asilimia 111 Liberia.