Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais wa zamani wa Guinea kushtakiwa, Bangura apongeza

Rais wa zamani wa Guinea kushtakiwa, Bangura apongeza

Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kingono Zainab Hawa Bangura amekaribisha kutangazwa kwa mashitaka dhidi ya Rais wa zamani wa Jamhuri ya Guinea Moussa Dadis Camara kufuatia uchunguzi wa matukio ya ukatili wa kingono ya mwaka 2009. Taarifa zaidi na John Kibego.

 (Taarifa zaidi na John kibego.)

 Bi. Bangura amesifu mamlaka zote kwa kuonyesha umiliki, uongozi na uwajibikaji katika mchakato unaosaka kuwajibisha watekelezaji wa ukatili uliyoshuhudiwa na ulimwengu ukitendeka mjini Conakry.

 Amesema mashitaka dhidi Rais huyo wa zamani yanawakilisha hatua muhimu za serikali ya Guinea katika kupambana na ukatili uliotendwa kuambatana na jinai dhidi ya wathiriwa ambao majina yao yamehifadhiwa.

 Moussa Dadis Camara alikuwa Rais wa Guinea wakati ukatili huo ulipotendeka tarehe 28 Septemba mwaka 2009.

 Tume ya Uchunguzi ya Kimataifa iliyoongozwa na Umoja wa Mataifa ilibaini kwamba angalau watu 156 waliuawa, wanawake na wasichana 109 walibakwa na kukumbwa na aina mbalimbali za ukatili wa kingono na watu wengine 1,000 kujeruhiwa katika kutokana na matukio kwenye medani na maeneo jirani..

Tangu mwaka 2011, Jopo la majaji likisaidia na watalamu wa Umoja wa Mataifa limefungua mashitaka dhidi ya watu 15 wakiwemo  maafisa wa ngazi ya juu jeshini.